Saturday, July 6, 2013

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA YATANGAZA TAREHE YA KUANZA KWA MABARAZA YA KATIBA

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ametangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya wilaya, huku akiwaonya watu wa kada mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa kutokuingilia mikutano hiyo.
Vilevile Jaji Warioba alieleza sababu za Tume hiyo kupendekeza Serikali tatu, huku akisisitiza kuwa suala hilo lilikuwepo tangu siku nyingi na Tume iliamua kupendekeza Serikali tatu kwa kuwa ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuulinda muungano.
Kauli hiyo inaonekana kama kukijibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimependekeza kuwepo kwa Serikali mbili, ikiwa ni siku chache baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Katiba.
Mikutano hiyo inafanyika baada ya Juni 3 mwaka huu, Tume hiyo kutoa rasimu ya Katiba na kusambaza katika vijiji, mitaa na shehia kwa ajili ya kujadiliwa na wananchi, ambao nao watachangia mawazo yao kwa wawakilishi wao waliowachagua kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, inaeleza kuwa mikutano hiyo itaanza Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu na kutakuwa na jumla ya Mabaraza 177, Tanzania Bara 164 na Zanzibar 13.
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa mapendekezo yake yanapitishwa huku kikitumia wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wakiwemo wa ngazi ya mtaa, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akiwaeleza wajumbe wa mabaraza ya Katiba jijini Dar es Salaam juzi azma ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.
Wakati CCM wakieleza hayo, Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana leo na kesho katika kikao cha dharura jijini Dar es Salaam ili kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anayemaliza muda wake, Profesa Issa Shivji, Juni 21 mwaka huu alisema kama Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano ikikubaliwa bila mabadiliko makubwa itasababisha kuvunjika kwa Muungano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema hairuhusiwi kwa makundi, vyama vya siasa au mtu yeyote kuingia katika mabaraza hayo kwa lengo la kushawishi kukubaliwa na maoni ya aina fulani. Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na gazeti hili, juu ya taarifa zilizopo kwamba baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeandaa rasimu zao kwa lengo la kuwashawishi wajumbe wa mabaraza kupitisha maoni yao.
“Mikutano na Mabaraza ya Katiba siyo ya kupiga kura bali ni kujadili na kutoa hoja ambazo zitakuwa na msingi kwa masilahi ya taifa na siyo kutetea masilahi ya kundi au watu fulani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza;
“Hilo la vyama kuandaa rasimu zao kwa lengo la kuingilia utaratibu huu sijalisikia, ila kikubwa ni kwamba si ruhusa kuingilia mchakato huu kwa sababu utafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” alisema Warioba na kusisitiza; “Wananchi watoe maoni ambayo yatasaidia kuiboresha rasimu iliyotolewa kwa kuweka mbele masilahi ya taifa na kuepuka ubinafsi wa mtu mmojammoja au makundi ya aina yeyote.”
Alisema Tume yake itapokea maoni na mapendekezo yote ambayo yatakuwa na lengo la kuiboresha rasimu ambayo itaweka umoja wa kitaifa na siyo kuwagawa Watanzania.

CHANZO: MWANANCHI